Last Updated on 21/09/25 by Tabibu Fadhili Paulo
Usile vyakula vifuatavyo kama unaumwa Bawasiri
Unapoumwa bawasiri unapaswa kuwa makini sana juu ya chakula unachokula na vinywaji unavyokunywa kila siku kwani vinao uwezo wa kurahisisha au kukwamisha matibabu kwako.
Siri iliyopo katika kupunguza au kuitibu bawasiri ipo kwenye vyakula hasa vyakula ambavyo vinaweza kukusaidia usipate choo kigumu au usikose kabisa choo.
Usikubali siku nzima ipite hujapata choo japo mara moja.
Mtu mwenye afya nzuri anatakiwa apate choo mara mbili mpaka tatu ndani ya masaa 24.
Siri ipo hapo.
Kwa sababu hiyo, nimekuandalia maelezo haya juu ya vyakula na vinywaji ambavyo itakulazimu uvikwepe ili uweze kupona bawasiri haraka na kwa urahisi zaidi.
Epuka vyakula vifuatavyo kama unaumwa bawasiri:
1. Vyakula vya kusisimua (Spicy foods):
Kama umekuwa ukisumbuliwa na bawasiri na kufunga choo au umekuwa ukipata choo kigumu kwa kipindi kirefu kuna uwezekano mkubwa umekuwa ukila vyakula vyenye kusisimuwa.
Kama una bawasiri vyakula vya kusisimuwa ni adui mkubwa kwako na unatakiwa uviache haraka ili kunusuru afya yako na uweze kupata kupona bawasiri.
Vyakula vya kusisimua ni pamoja na ketchup, chill sauce, tomato sauce, achali, pilipili na vingine vingi vya jamii hii.
Mwili wako utakushukuru sana kwa uamuzi huu wa kusitisha kutumia vyakula hivi.
2. Baadhi ya bidhaa zitokanazo na maziwa:
Kama una bawasiri huna tofauti sana na mtu mwenye vidonda vya tumbo na mara nyingi vitu hufuatana au huwa pamoja.
Kama ilivyo kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo kwamba hatakiwi kupendelea kunywa maziwa fresh basi hata wewe mwenye bawasiri usinywe maziwa fresh na jibini (cheese).
Maziwa na jibini vinaweza kukuongezea aside tumboni mwako na kuleta shida au usumbufu zaidi kama una bawasiri.
Unaweza kutumia vyakula hivi pengine mara moja tu kwa wiki na siyo kila siku.
3. Nyama nyekundu:
Ukiacha vyakula vya kusisimua kitu kingine kinachoweza kuongeza maumivu zaidi au kuchelewesha kupona kwa bawasiri ni ulaji wa nyama hasa nyama nyekundu.
Ukiwa na bawasiri maana yake mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula haupo sawa na haufanyi kazi kwa kiwango chake kama unavyotakiwa.
Na moja ya vyakula vyenye shida kwenye kumeng’enywa tumboni ni nyama nyekundu yaani nyama ya ng’ombe na nyama ya mbuzi.
Kama unahitaji sana kula nyama napendekeza ule mara 1 tu kwa wiki na uepuke kwa gharama nyama choma na mishikaki.
Unaweza kula samaki au nyama ya kuku wa kienyeji mara kwa mara.
Ukiona unakosa choo au unapata choo kigumu mara kwa mara badili mlo wako kwa siku kadhaa na ule mboga za majani, matunda na maji tu.
4. Pombe:
Siyo jambo baya kupata bia moja au glasi mbili za mvinyo mwekundu mara moja moja au siku za wikendi.
Hata hivyo kama wewe ni wale ambao haiwezi kupita siku bila kunywa pombe basi itakuwa vigumu kwako kupona bawasiri.
Pombe ina kawaida ya kukausha maji mwilini na mgonjwa wa bawasiri unahitaji sana maji mwilini mwako kuliko kitu kingine chochote.
Maji yanapopungua mwilini matokeo yake ni kukosa choo au kupata choo kigumu na kuongezeka zaidi na zaidi kwa ugonjwa badala ya kupona.
5. Vyakula vya viwandani na vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi:
Watu wengi wanaofanya kazi maofisini wanalazimika kula migahawani au kwenye maduka na vingi ya vyakula hivyo huwa si salama kwa mtu mwenye bawasiri.
Unahitaji kula vyakula vya asili zaidi unapougua bawasiri na utatakiwa uachane kabisa na vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi kama vile chips, maaandazi na vingine vyote vinavyopikwa kwa staili hii ya kuwa katikati ya mafuta mengi.
6. Kaffeina:
Habari mbaya kwa wale wenzangu wapenda kahawa na chokoleti!
Kaffeina inajulikana kwa kusababisha maumivu na upungufu wa maji mwilini.
Kama una bawasiri nakushauri uache vitu hivi haraka navyo ni chai ya rangi, kahawa, chokoleti na soda zote.
Kama ni chai jaribu chai ya mchaichai na utumie asali badala ya sukari mara zote.
Unapoumwa au uanzapo tu kuona dalili za bawasiri ndiyo wakati muafaka wa kutafuta dawa na matibabu mapema.
Usisubiri mpaka tatizo liwe sugu au kubwa ndiyo uanze kutafuta dawa kwani hiyo itakupelekea kupona kwako kuchukuwe muda mrefu zaidi.
Naitwa Fadhili Paulo ni Tabibu wa tiba asili, nauza dawa za Asili, Nipo Kibugumo Mji Mwema Kigamboni Dar Es Salaam
Kama umependezwa na makala hii tumia batani za kijamii hapa chini share na wengine uwapendao.